Tuesday, January 10, 2012

Swahili Center yamtunikia Dr. Karume nishani ya ‘Shujaa wa Zanzibar’ ikiwa ni hatua ya mwisho ya 100% Zanzibari


Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe, Dk. Amani Karume akipokea nishani ya "Shujaa wa Zanzibar" kutoka kwa Mzee Hassan Nassor Moyo. Wakishuhudia makabidhiano hayo ni Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Mhe. Ismail Jussa (kulia) na Kheri Jumbe ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Swahili Center.
Rais Mstaafu Mhe. Dk. Karume akiwa na ujumbe ulimtembelea. Kutoka Kushoto ni Mahsin Basalama (Mkurugenzi wa Sanaa/ Swahili Center), Mhe. Ismail Jussa, Mzee Hassan Nassor Moyo, Kheri Jumbe na Abbas Kadhim (Mdau wa Swahili Center)

Kituo cha Sanaa za Maonesho za Waswahili (Swahili Performing Arts Center)
Zanzibar kimemtunukia Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Dr. Amani Karume,
nishani ya ‘Shujaa wa Zanzibar’ ikiwa ni hatua ya mwisho katika
kuadhimisha kufikiwa kwa maridhiano na hatimaye serikali ya umoja wa
kitaifa nchini Zanzibar.

Dr. Karume alikabidhiwa nishani hiyo na mwanasiasa mkongwe Mzee Hassan
Nassor Moyo  siku ya Ijumaa tarehe 23 Desemba 2011 katika hafla fupi
iliyofanyika nyumbani kwake huko Mbweni nje kidogo ya Mji Mkongwe.

Akiwasilisha risala yake katika tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Swahili
Performing Arts Center Kheri Jumbe alitoa shukrani kwa Dr. Karume kutokana
na jitihada zake katika kuleta amani ya kudumu nchini Zanzibar.

Jumbe alieleza kuwa, taasisi yake iliona umuhimu wa kuandaa sherehe za
maridhiano kupitia mradi wa sanaa uliopewa utambulisho wa 100%  Zanzibari
(Mzanzibari asilimia moja) ili kuwaenzi waasisi wa maridhiano hayo na
kueliimisha wananchi juu ya umuhimu wake.

“Kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia Oktoba 4 hadi Desemba 3, tumekwenda
katika mikoa yote ya Zanzibar na kuwasilisha ujumbe juu ya umuhimu wa
kuimarisha misingi ya umoja na kuweka mbele uzalendo, ‘ alisema Jumbe.

Akikabidhi nishani hiyo kwa Rais mstaafu huyo, Mzee Hassan Nassor Moyo alirejea
wasia wake wakutaka viongozi wakuu wa Zanzibar kutowavumulia watendaji wa
serikali wanaovuruga maridhiano.

Katika kuipokea nishani hiyo, Dr. Karume aliwapongeza watendaji wa Swahili
Center pamoja na wasanii walioshirki katika mradi huo kwa juhudi zao
katika kuyaendeleza maridhiano kupitia sanaa zilizobeba ujumbe huo.

Nishani kama hiyo ya ‘shujaa wa Zanzibar’ alitunukiwa pia Makamo wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad katika kilele cha
sherehe za maridhiano huko uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba tarehe 3
Desemba 2011. 
 
Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif akipokea nishani ya "Shujaa wa Zanzibar" katika kilele cha sherehe za 100% Zanzibari: Shangwe za Maridhiano na Umoja wa Kitaifa
Wengine waliohudhuria katika uwasilishwaji wa nishani hiyo kwa Dr. Karume
ni Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Mhe Ismail Jussa pamoja na
Mkurugenzi wa Sanaa was Swahili Center, Mahsin Basalama.

Kupitia mradi wa 100% Zanzibari wasanii 130 kutoka vikundi 11 vya sanaa za
maonesho walishiriki katika kambi za kjenga umoja na kufanya maonesho
nchini kote.

Mradi wa 100% Zanzibari umedhaminiwa na Ubalozi wa Norway pamoja na
kampuni ya mawasiliano ya Zantel.

No comments:

Post a Comment