Tuesday, February 14, 2012

MKOTA NA JUHUDI WAWAKILISHA PEMBA KTK BUSARA

Kundi la Juhudi Taarab la Chake-Chake wakitumbuiza ktk Sauti za Busara

Mkota Spirit Dancers wakitawala jukwaa siku ya ufungzi wa Busara 2012

Bosso la chambi laivu ndani ya Ngome Kongwe kutoka kwa Mkota
Wiki iliyopita Swahili Center ilifanikiwa kutimiza azma yake ya kuongeza uwakilishi wa sanaa za Zanzibar katika matamasha yanayofanyika Zanzibar kwa kuvileta vikundi viwili kutoka Pemba. Vikundi vilivyowakilisha sanaa za maonesho za asili za Zanzibar katika tamasha la Sauti za Busara la 2012 ni Mkota Spirit Dancers kutoka Mkoani na Juhudi Taarab kutoka Chake-Chake.

Uwakilishi wa vikundi hivyo kupitia Swahili Center umewezeshwa kwa ufadhili wa kampuni ya safari za anga ya hapa Zanzibar, ZanAir Ltd, ambayo mwaka huu inasherehekea miaka 20 ya utaoji huduma tangu kuanzishwa 1992

Katika tamasha hilo, kundi la Mkota Spirit Dancers waliwatangulia Juhudi Taarab kwa kufanya oehso lao tarehe 9 February katika ukumbi wa Mambo Club, ndani ya Ngome Kongwe. Wakiwa wamepangiwa kutumbuiza katika siku hiyo ya ufunguzi, kundi hilo liliacha maji katika jukwaa kufuatia shoo yao ya ngoma ya Kumbwaya.

Juhudi Taarab nao walipata fursa ya kuonesha kilichowawezesha kuwepo katika 'gemu' kwa zaidi ya miaka 70 kwa kuja jukwaani siku ya Jumamosi tarehe 11 Februari na kuwalemaza wapenzi wa Taarab asilia kwavibao vyao kama vile 'Vijumbajumba' iliyiombwa na mtunzi wake Malik Hamad 'Wastara'. Isitoshe, mkali wa shairi la 'Bora Niombe', Ali Said 'Wazera' pia alikuwa jukwaani na kuimba 'Karamu' huku wapenzi wake wakiserebuka pembezoni mwa jukwaa.

Kwa ujumla, kuwepo kwa Mkota Spirit Dancers na Juhudi katika tamasha la mwaka huu la Sauti za Busara ni sehemu muhimu  katika kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa Swahili Center mwaka jana. Kutokana na hilo, ni matumaini yetu kuwa maonesho ya vikundi hivyo kutoka hapa nyumbani, yaliyokuwa na ubora wa hali ya juu, yameonekana na kuwa huenda ikiwa ndiyo mwanzo wa vikundi hivyo kupata ajira wanazostahili.

Swahili Center inapenda kutoa shukrani za dhati kwa kampuni ya ZanAir kwa ukarimu wake na kwa Busara Promotions kwa mashirikiano mazuri baina ya taasisi zetu.

Watendaji wa Swahili Center wakiwa na Mkurugenzi wa Busara, Yusuf Mahmoud

 
Mdau Salma Said akiwa na kundi la Mkota Ngoma (pembeni: Mahsin)
Watendaji wa Swahili Center wakiwa na kundi la Juhudi kufuatia onesho lao







Wednesday, January 25, 2012

SEARCH FOR COMMON GROUND WAITEMBELEA CENTER


Kutoka Kushoto: Bi Marks, Mahsin, Kheri na Bi Manirakiza

Watendaji kutoka taasisi ya Search for Common Ground yenye makaomakuu yake nchini Marekani, leo walitembelea ofisi ya Swahili Center katika jitihada za kuimarisha mahusiano baina ya asasi mbili hizo za kiraia.

Katika ujuio huo, taasisi ya Search for Common Ground iliwakilishwa na Bi Susan  Collin Marks ambaye ni Senior Vice President wa taasisi hiyo pamoja na Bi Spes Manirakiza ambaye ndiye atakayekuwa Mkrugenzi wa taasisi hiyo katika ofisi yao mpya iliyopo Zanzibar.
Wakati wa ziara hiyo ya kirafiki, wageni kutoka Search for Common Ground walipata fursa ya kupitia tathmini juu ya mradi wa 100% Zanzibari uliofanyika kuanzia mwezi wa Oktoba hadi Desemba 2011 kutoka kwa watendaji wa Swahili Center.
Akiwapokea wageni hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Swahili Center, Kheri Jumbe, aliwatambulisha mafanikio pamoja na changamoto zilizojiri katika utekelezaji wa mradi wa 100% Zanzibari uliokuwa na malengo ya kuimarisha misingi ya maridhiano na umoja wa kitaifa wa Zanzibar.  Search for Common Ground ni taasisi iliyojikita katika kuwezesha jamii tofauti ulimwenguni kufikia maafikiano ya kuleta amani endelevu.
Akipokea tathmini hiyo, Bi Susan Collin Marks alipongeza upeo na  juhudi za Swahili Center katika kubuni mradi wa 100% Zanzibari na kuutekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu licha ya changamoto zilizojitokeza. Pia aliwataka watendaji wa taasisi hiyo kuendelea kutumia vyema jukwaa la sana za maonesho katika kujenga umoja na mshikamano baina ya wananchi wa Zanzibar mbali na malengo mengine ya kazi za taasisi hiyo changa.
“Ni jambo la kupigiwa mfano kutokana na mabadiliko yaliyopatikana Zanzibar katika kipindi kifupi cha maridhiano ya kisiasa yaliyoafiiwa nchini kwenu,’ alisema Bi Marks. ‘Kilichobaki sasa ni kuyazalisha matunda ya matumaini hayo mapya na kuyafanya yenye manufaa na kiuchumi na kijamii kwa waZanzibari.’
Kwa upande wa Bi Manirakiza, yeye aliwaahidi watendaji wa Swahili Center kuwa akiwa Mkrugenzi wa taasisi hiyo hapa Zanzibar atajitahidi kadiri ya uwezo wake katika kufanya kazi na Swahili Center pamoja na kuwashiriisha wasanii katika miradi ya Search for Common Ground nchini Tanzania.
Ujio wa Search for Common Ground katika ofisi ya Swahili Center ni marejeo ya ziara ya kirafiki iliyofanywa na Mkurugenzi wa Swahili Center mwaka jana katika ofisi za Search for Common Ground iliyopo mjini Washington DC, Marekani.

Search for Common Ground - www.sfcg.org


Wednesday, January 18, 2012

ZANAIR YAIPIGA JEKI SWAHILI CENTER KUSHIRIKI BUSARA

Watendaji wa Swahili Center, wakiwa na Meneja Mauzo na Masoko wa Kampuni ya ZanAir Bw. Ashish Nagewadia (Kushoto) pamoja na Reservations Supervisor Asya Abdulla (Wa Pili kutoka Kulia)

Kituo cha Swahili Center kimeingia makubaliano ya mashirikiano na mdau wa sanaa nchini, Busara Promotions, utakaotoa fursa ya kushiriki katika tamasha la Sauti za Busara la 2012 kwa njia maalum.

Makubaliano hayo yamelenga kuipa fursa Swahili Center kudhamini vikundi viwili vya sanaa kutoka kisiwani Pemba kutoa burdani katika tamasha hilo litakalofanyika kuanzia tarehe 8 hadi 12 Februari 2012. Katika makubaliano hayo, Swahili Center itashirikiana na kampuni ya ndege ya ZanAir katika kuviwezesha vikundi vya Mkota 'Spirit Dancers' na Juhudi Taarab kushiriki katika tamasha.

Mkurugenzi wa Sanaa wa Swahili Center, Mahsin Basalama, ambaye ndiye mtekelezaji na msimamizi mkuu wa miradi yote kwa upande wa ubunifu alikaribisha fursa hiyo kwa kusema kuwa kuvitangaza vikundi vinavyofanya sanaa zenye ubora wa hali ya juu ni mojawapo katika mikakati muhimu ya Swahili Center.

Mkurugenzi wa Sanaa wa Swahili Center, Mahsin Basalama (kushoto) akipokezana hati ya mashirikiano na Msaidizi Mkurugenzi wa Busara Promotions, Rosie Carter
Kwa upande wa ZanAir, Meneja wa Mauzo na Masoko, Ashish Nagewadia alisema kuwa ushiriki wao katika kuleta vikundi hivyo kutoka kisiwani Pemba ni njia mojawapo ya kampuni ya ZanAir kutoa shukrani kwa watu wa Pemba kwa kutumia huduma zao. Kampuni ya ZanAir inatimiza miaka 20 ya kutoa huduma za usafiri wa ndege tangu ilivyoanzishwa mwaka 1992.

Taarifa kamili kuhusu makubaliano hayo zitatolewa rasmi baada ya kukamilika mipango husika ikiwemo kutangazwa kwa mfadhili wa mashirikiano hayo.

ZANAIR LTD - CELEBRATING 20 YEARS OF SERVICE

Tuesday, January 10, 2012

Swahili Center yamtunikia Dr. Karume nishani ya ‘Shujaa wa Zanzibar’ ikiwa ni hatua ya mwisho ya 100% Zanzibari


Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe, Dk. Amani Karume akipokea nishani ya "Shujaa wa Zanzibar" kutoka kwa Mzee Hassan Nassor Moyo. Wakishuhudia makabidhiano hayo ni Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Mhe. Ismail Jussa (kulia) na Kheri Jumbe ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Swahili Center.
Rais Mstaafu Mhe. Dk. Karume akiwa na ujumbe ulimtembelea. Kutoka Kushoto ni Mahsin Basalama (Mkurugenzi wa Sanaa/ Swahili Center), Mhe. Ismail Jussa, Mzee Hassan Nassor Moyo, Kheri Jumbe na Abbas Kadhim (Mdau wa Swahili Center)

Kituo cha Sanaa za Maonesho za Waswahili (Swahili Performing Arts Center)
Zanzibar kimemtunukia Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Dr. Amani Karume,
nishani ya ‘Shujaa wa Zanzibar’ ikiwa ni hatua ya mwisho katika
kuadhimisha kufikiwa kwa maridhiano na hatimaye serikali ya umoja wa
kitaifa nchini Zanzibar.

Dr. Karume alikabidhiwa nishani hiyo na mwanasiasa mkongwe Mzee Hassan
Nassor Moyo  siku ya Ijumaa tarehe 23 Desemba 2011 katika hafla fupi
iliyofanyika nyumbani kwake huko Mbweni nje kidogo ya Mji Mkongwe.

Akiwasilisha risala yake katika tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Swahili
Performing Arts Center Kheri Jumbe alitoa shukrani kwa Dr. Karume kutokana
na jitihada zake katika kuleta amani ya kudumu nchini Zanzibar.

Jumbe alieleza kuwa, taasisi yake iliona umuhimu wa kuandaa sherehe za
maridhiano kupitia mradi wa sanaa uliopewa utambulisho wa 100%  Zanzibari
(Mzanzibari asilimia moja) ili kuwaenzi waasisi wa maridhiano hayo na
kueliimisha wananchi juu ya umuhimu wake.

“Kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia Oktoba 4 hadi Desemba 3, tumekwenda
katika mikoa yote ya Zanzibar na kuwasilisha ujumbe juu ya umuhimu wa
kuimarisha misingi ya umoja na kuweka mbele uzalendo, ‘ alisema Jumbe.

Akikabidhi nishani hiyo kwa Rais mstaafu huyo, Mzee Hassan Nassor Moyo alirejea
wasia wake wakutaka viongozi wakuu wa Zanzibar kutowavumulia watendaji wa
serikali wanaovuruga maridhiano.

Katika kuipokea nishani hiyo, Dr. Karume aliwapongeza watendaji wa Swahili
Center pamoja na wasanii walioshirki katika mradi huo kwa juhudi zao
katika kuyaendeleza maridhiano kupitia sanaa zilizobeba ujumbe huo.

Nishani kama hiyo ya ‘shujaa wa Zanzibar’ alitunukiwa pia Makamo wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad katika kilele cha
sherehe za maridhiano huko uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba tarehe 3
Desemba 2011. 
 
Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif akipokea nishani ya "Shujaa wa Zanzibar" katika kilele cha sherehe za 100% Zanzibari: Shangwe za Maridhiano na Umoja wa Kitaifa
Wengine waliohudhuria katika uwasilishwaji wa nishani hiyo kwa Dr. Karume
ni Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Mhe Ismail Jussa pamoja na
Mkurugenzi wa Sanaa was Swahili Center, Mahsin Basalama.

Kupitia mradi wa 100% Zanzibari wasanii 130 kutoka vikundi 11 vya sanaa za
maonesho walishiriki katika kambi za kjenga umoja na kufanya maonesho
nchini kote.

Mradi wa 100% Zanzibari umedhaminiwa na Ubalozi wa Norway pamoja na
kampuni ya mawasiliano ya Zantel.