Monday, November 21, 2011

NADI IKHWAN SAFAA, JUHUDI TAARAB ZAITEKA KISONGE



Wananchi wakiwa wametulia wakikongwa nyoyo zao na wasanii.

MAONESHO ya Taarab kushangilia maridhiano ya kisiasa Zanzibar, juzi yalihamia katika Uwanja wa Kisonge, ambapo vikundi vya nadi Ikhwan Safaa na Juhudi kutoika Chake Chake, Pemba viliwapa uhondo mashabiki wengi waliojimwaga kiwanjani hapo.

Tamasha hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Swahili Performing Arts, lilivutia wapenzi wengi kutokana na nyimbo murua zilizoporomoshwa na waimbaji magwiji wa vikundi hivyo.

kundi la Juhudi ambalo lilikuwa la kwanza kupanda jukwaani, lilimudu vyema kuzikonga nyoyo za wananchi kwa nyimbo zao tamu kama vile 'Yatima', 'Zimekwisha enzi zako', 'Mshikamano' na Bora niombe' uliowavutia wangi.

Bibie Saada Mohammed Akighani wimbo wa Njangu.

Nalo kundi la Nadi Ikhwan Safaa liliamsha hisia za hadhira iliyofurika uwanjani hapo, kwa nyimbo za 'Wadhanifu' ulioghaniwa na mkongwe Sihaba Juma, 'Njangu' (Saada Mohammed), 'Hakika nnakupenda' (Ally Massoud)

Vibao vingine vilivyowazingua wapenzi ni 'Naomba kwako bibie'(Sameer Basalama),'Namuenzi'(Faudhia Abdullah), ambazo ziliwaibua washabiki kila mara katika viti vyao na kuungana pamoja kuserebuka.

Aidha wasanii wa vikundi hivyo kwa pamoja waliimba wimbo wa kusisitiza kuuendeleza muafaka na maridhiano kati ya wananchi wa Zanzibar, ukiwemo wimbo wa 'Maridhiano' (Faudhia Abdullah).

'Usiyalaumu macho' Mr. Wazera aliwakuna wananchi.

Msanii wa siku nyingi Sihaba Juma, alirudi tena jukwaani kugani wimbo 'Nnazama', klabu Wazera hajaonesha majojo majojo yake katika wimbo 'Usijalaumu macho', na Saada Muhammed akahitimisha onesho hilo kwa kibao 'Leo tena'.
Tamasha hilo limepangwa kuendelea tena Jumamosi ijayo katika ukumbi wa Ngome Kongwe, ambapo kundi la ' Unguja All Stars Taarab' na kikundi cha ngoma za asili 'Mkota' kutoka Mkoani Pemba vitatoa burdani mwanana. 

Ma mia ya watu walirindima katika uwanja wa kisonge.

No comments:

Post a Comment