Wednesday, January 18, 2012

ZANAIR YAIPIGA JEKI SWAHILI CENTER KUSHIRIKI BUSARA

Watendaji wa Swahili Center, wakiwa na Meneja Mauzo na Masoko wa Kampuni ya ZanAir Bw. Ashish Nagewadia (Kushoto) pamoja na Reservations Supervisor Asya Abdulla (Wa Pili kutoka Kulia)

Kituo cha Swahili Center kimeingia makubaliano ya mashirikiano na mdau wa sanaa nchini, Busara Promotions, utakaotoa fursa ya kushiriki katika tamasha la Sauti za Busara la 2012 kwa njia maalum.

Makubaliano hayo yamelenga kuipa fursa Swahili Center kudhamini vikundi viwili vya sanaa kutoka kisiwani Pemba kutoa burdani katika tamasha hilo litakalofanyika kuanzia tarehe 8 hadi 12 Februari 2012. Katika makubaliano hayo, Swahili Center itashirikiana na kampuni ya ndege ya ZanAir katika kuviwezesha vikundi vya Mkota 'Spirit Dancers' na Juhudi Taarab kushiriki katika tamasha.

Mkurugenzi wa Sanaa wa Swahili Center, Mahsin Basalama, ambaye ndiye mtekelezaji na msimamizi mkuu wa miradi yote kwa upande wa ubunifu alikaribisha fursa hiyo kwa kusema kuwa kuvitangaza vikundi vinavyofanya sanaa zenye ubora wa hali ya juu ni mojawapo katika mikakati muhimu ya Swahili Center.

Mkurugenzi wa Sanaa wa Swahili Center, Mahsin Basalama (kushoto) akipokezana hati ya mashirikiano na Msaidizi Mkurugenzi wa Busara Promotions, Rosie Carter
Kwa upande wa ZanAir, Meneja wa Mauzo na Masoko, Ashish Nagewadia alisema kuwa ushiriki wao katika kuleta vikundi hivyo kutoka kisiwani Pemba ni njia mojawapo ya kampuni ya ZanAir kutoa shukrani kwa watu wa Pemba kwa kutumia huduma zao. Kampuni ya ZanAir inatimiza miaka 20 ya kutoa huduma za usafiri wa ndege tangu ilivyoanzishwa mwaka 1992.

Taarifa kamili kuhusu makubaliano hayo zitatolewa rasmi baada ya kukamilika mipango husika ikiwemo kutangazwa kwa mfadhili wa mashirikiano hayo.

ZANAIR LTD - CELEBRATING 20 YEARS OF SERVICE

1 comment: