Kutoka Kushoto: Bi Marks, Mahsin, Kheri na Bi Manirakiza |
Watendaji kutoka taasisi ya Search for Common Ground yenye
makaomakuu yake nchini Marekani, leo walitembelea ofisi ya Swahili Center
katika jitihada za kuimarisha mahusiano baina ya asasi mbili hizo za kiraia.
Katika ujuio huo, taasisi ya Search for Common Ground
iliwakilishwa na Bi Susan Collin Marks
ambaye ni Senior Vice President wa taasisi hiyo pamoja na Bi Spes Manirakiza
ambaye ndiye atakayekuwa Mkrugenzi wa taasisi hiyo katika ofisi yao mpya
iliyopo Zanzibar.
Wakati wa ziara hiyo ya kirafiki, wageni kutoka Search for
Common Ground walipata fursa ya kupitia tathmini juu ya mradi wa 100% Zanzibari
uliofanyika kuanzia mwezi wa Oktoba hadi Desemba 2011 kutoka kwa watendaji wa
Swahili Center.
Akiwapokea wageni hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Swahili
Center, Kheri Jumbe, aliwatambulisha mafanikio pamoja na changamoto zilizojiri
katika utekelezaji wa mradi wa 100% Zanzibari uliokuwa na malengo ya kuimarisha
misingi ya maridhiano na umoja wa kitaifa wa Zanzibar. Search for Common Ground ni taasisi
iliyojikita katika kuwezesha jamii tofauti ulimwenguni kufikia maafikiano ya
kuleta amani endelevu.
Akipokea tathmini hiyo, Bi Susan Collin Marks alipongeza upeo
na juhudi za Swahili Center katika
kubuni mradi wa 100% Zanzibari na kuutekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu licha
ya changamoto zilizojitokeza. Pia aliwataka watendaji wa taasisi hiyo kuendelea
kutumia vyema jukwaa la sana za maonesho katika kujenga umoja na mshikamano
baina ya wananchi wa Zanzibar mbali na malengo mengine ya kazi za taasisi hiyo changa.
“Ni jambo la kupigiwa mfano kutokana na mabadiliko
yaliyopatikana Zanzibar katika kipindi kifupi cha maridhiano ya kisiasa
yaliyoafiiwa nchini kwenu,’ alisema Bi Marks. ‘Kilichobaki sasa ni kuyazalisha
matunda ya matumaini hayo mapya na kuyafanya yenye manufaa na kiuchumi na
kijamii kwa waZanzibari.’
Kwa upande wa Bi Manirakiza, yeye aliwaahidi watendaji wa
Swahili Center kuwa akiwa Mkrugenzi wa taasisi hiyo hapa Zanzibar atajitahidi
kadiri ya uwezo wake katika kufanya kazi na Swahili Center pamoja na
kuwashiriisha wasanii katika miradi ya Search for Common Ground nchini
Tanzania.
Ujio wa Search for Common Ground katika ofisi ya Swahili
Center ni marejeo ya ziara ya kirafiki iliyofanywa na Mkurugenzi wa Swahili
Center mwaka jana katika ofisi za Search for Common Ground iliyopo mjini
Washington DC, Marekani.
Search for Common Ground - www.sfcg.org
No comments:
Post a Comment