Sherehe
za maridhiano na umoja wa kitaifa zilizoandaliwa na taasisi ya Swahili Center
zinaendelea kwa kasi ambapo kwa Ijumaa iliyopita, vikundi vya Nyota ya Umoja
(Maigizo,Nungwi) na Mkota Ngoma (Mkoani, Pemba) vilirindima katika kijiji cha
Nungwi, Unguja.
Katika
onesho hilo ambalo lilifanyika katika Uwanja wa Skuli ya Nungwi, Wilaya ya
Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, wapenzi wa fani za sanaa za maonesho
kutoka sehemu mbali mabli waliliminika na kujimwaga katika burudani hizo
zilizoanza saa 10 alasiri.
Kundi
la Maigizo la Nyota ya Umoja, maarufu kwa michezo yao kama vile ‘Dhulma Kafara’
na ‘Masikini naye Mtu’, walitoa burudani safi kupitia mchezo wa ‘Mchelea Mwana
Kulia’ uliobeba maudhui ya umuhimu wa ushirikiano wa kuyalinda maadili ya
KiZanzibari ndani ya jamii.
Nalo
kundi la Mkota Ngoma kutoka Mkoani, walikonga nyoyo za wapenzi wa Ngoma na asili
kwa kupiga ngoma zao za Msembwe, Unjunguu na Kumbwaya. Wengi waliohudhiria
shehere hizo walivutiwa sana na umahiri wa kundi hilo katika kuzicheza Ngoma
hizo.
Katika
kuutambulisha mradi huo kwa waliohudhuria onesho hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa
Swahili Center Bw. Kheri Abdalla Yussuf, aliwajulisha wapenzi hao wa sanaa za
utamaduni kuwa dhamira ya mradi huo ni kuimarisha misingi ya umoja wa kitaifa
nchini Zanzibar kupitia sanaa za utamaduni zenye burudani na mafunzo kwa jamii
yote.
Wakati
huo huo, aliyekuwa mgeni rasmi katika onesho hilo, Mhe. Bi Riziki Juma Simai
(Mkuu wa Wilaya ya Kasakazi A) aliwataka wananchi wa Nungwi na wote
waliohudhuria kuimarisha misingi ya umoja wa kitaifa kwa
vitendo.
Mradi
wa 100% Zanzibari (tafsiri; Mzanzibari asilimia mia moja) umekuwa ukifanya
maonesho katika Mikoa ya Unguja na Pemba kufuatia kambi za kisanii
zinazoshirikisha fani za Taarab, Ngoma za Utamaduni na michezo ya Kuigiza.
Shangwe hizo zimekuwa zikifanyika kwa awamu katika sehemu mbali mbali ambapo kwa
kipindi cha Nov 15-19 zitahamia katika Mkoa wa Mjini Maghribi.
Swahili
Performing Arts Center
(Kituo cha Sanaa za Maonesho cha Waswahili) ni taasisi ya iliyoanzishwa kwa
dhamira ya kuchangia katika maendeleo ya sanaa za maonesho asilia za Zanzibar
pamoja na zile za mwambao wa Waswahili kupitia uwezeshaji (wasanii), uzalishaji
wa kazi za sanaa, maonesho na ushirikishaji jamii. Dira ya Swahili Center ni
kuurejeshea hadhi utambulisho wa utamaduni wa Kiswahili.
Mradi
wa 100% Zanzibari umedhaminiwa na Ubalozi wa Norway pamoja na kampuni ya
mawasiliano ya Zantel.
No comments:
Post a Comment