Tuesday, February 14, 2012

MKOTA NA JUHUDI WAWAKILISHA PEMBA KTK BUSARA

Kundi la Juhudi Taarab la Chake-Chake wakitumbuiza ktk Sauti za Busara

Mkota Spirit Dancers wakitawala jukwaa siku ya ufungzi wa Busara 2012

Bosso la chambi laivu ndani ya Ngome Kongwe kutoka kwa Mkota
Wiki iliyopita Swahili Center ilifanikiwa kutimiza azma yake ya kuongeza uwakilishi wa sanaa za Zanzibar katika matamasha yanayofanyika Zanzibar kwa kuvileta vikundi viwili kutoka Pemba. Vikundi vilivyowakilisha sanaa za maonesho za asili za Zanzibar katika tamasha la Sauti za Busara la 2012 ni Mkota Spirit Dancers kutoka Mkoani na Juhudi Taarab kutoka Chake-Chake.

Uwakilishi wa vikundi hivyo kupitia Swahili Center umewezeshwa kwa ufadhili wa kampuni ya safari za anga ya hapa Zanzibar, ZanAir Ltd, ambayo mwaka huu inasherehekea miaka 20 ya utaoji huduma tangu kuanzishwa 1992

Katika tamasha hilo, kundi la Mkota Spirit Dancers waliwatangulia Juhudi Taarab kwa kufanya oehso lao tarehe 9 February katika ukumbi wa Mambo Club, ndani ya Ngome Kongwe. Wakiwa wamepangiwa kutumbuiza katika siku hiyo ya ufunguzi, kundi hilo liliacha maji katika jukwaa kufuatia shoo yao ya ngoma ya Kumbwaya.

Juhudi Taarab nao walipata fursa ya kuonesha kilichowawezesha kuwepo katika 'gemu' kwa zaidi ya miaka 70 kwa kuja jukwaani siku ya Jumamosi tarehe 11 Februari na kuwalemaza wapenzi wa Taarab asilia kwavibao vyao kama vile 'Vijumbajumba' iliyiombwa na mtunzi wake Malik Hamad 'Wastara'. Isitoshe, mkali wa shairi la 'Bora Niombe', Ali Said 'Wazera' pia alikuwa jukwaani na kuimba 'Karamu' huku wapenzi wake wakiserebuka pembezoni mwa jukwaa.

Kwa ujumla, kuwepo kwa Mkota Spirit Dancers na Juhudi katika tamasha la mwaka huu la Sauti za Busara ni sehemu muhimu  katika kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa Swahili Center mwaka jana. Kutokana na hilo, ni matumaini yetu kuwa maonesho ya vikundi hivyo kutoka hapa nyumbani, yaliyokuwa na ubora wa hali ya juu, yameonekana na kuwa huenda ikiwa ndiyo mwanzo wa vikundi hivyo kupata ajira wanazostahili.

Swahili Center inapenda kutoa shukrani za dhati kwa kampuni ya ZanAir kwa ukarimu wake na kwa Busara Promotions kwa mashirikiano mazuri baina ya taasisi zetu.

Watendaji wa Swahili Center wakiwa na Mkurugenzi wa Busara, Yusuf Mahmoud

 
Mdau Salma Said akiwa na kundi la Mkota Ngoma (pembeni: Mahsin)
Watendaji wa Swahili Center wakiwa na kundi la Juhudi kufuatia onesho lao